Thursday , 2nd Sep , 2021

Jeshi la Polisi limekamilisha upelelezi wa awali wa tukio la askari wake watatu pamoja na mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi, kuuawa kwa risasi na mtu aliyefahamika kama Hamza Mohammed katika eneo la Ubalozi wa Ufaransa uliopo Dar es Salaam, na kubaini Hamza alikuwa na viashiria vya ugaidi

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI Camilius Wambura

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI Camilius Wambura, amesema Hamza Mohammed alikuwa na viashiria vya ugaidi alivyovipata kupitia mafunzo ya mitandao ya kijamii ya ndani na nje ya nchi na alikuwa akiishi kisiri.

"Hamza Mohammed kwa kipindi kirefu amekuwa akijifunza mambo ya kigaidi kwa kuangalia mitandao ambayo inaonesha matendo ya Al Shabaab, ISIS na magaidi wengi hujifunza kupitia mitandao hiyo na alikuwa ni kigaidi wa kujitoa mhanga," amesema DCI Wambura.

Aidha, akizungumzia suala la Hamza kumiliki mgodi wa madini DCI Wambura amesema kuwa, "Hamza hakuwa na madini wala pesa na hakuwa katika nafasi yoyote ya kumiliki madini wala pesa licha ya kwamba watu wengi wameongea kwamba alikuwa anamiliki migodi ya madini kule Chunya uchunguzi wetu umebaini hali hiyo ya maisha ilikwisha”.