Wednesday , 6th Oct , 2021

Benki ya NBC na Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF zimeingia makubaliano ya Mkataba wa miaka mitatu ya udhamini wa Ligi Kuu Tanzania bara na msimu huu benki hiyo itatoa kitita cha Bilioni 2.5 kabla ya VAT.

Rais wa TFF, Wallace Karia akizungumza na Waandishi wa Habari

Akizungumza baada ya kuingia makubaliano hayo ,Rais Karia amesema wameingia makubaliano na NBC baada ya mchakato wa muda mrefu ambao ulikuwa na lengo la kuwekza vizuri katika mchezo wa mpira wa miguu.

Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF, Wallace Karia amesema kuanzia sasa Ligi Kuu inatambulika NBC Tanzania Premier League.

Karia amesema wamepata udhamini kutokana na Shirikisho lak kuaminiwa na taasisi mbalimbali kutokana na kuwa na Utawala bora pamoja na uadilifu katika rasilimali fedha na kuzipeleka katika maeneo yaliyoekezwa kwa maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu.

Ameongeza kuwa pesa hizo zinapelekwa katika Bodi ya Ligi, ambao ndio waendeshaji wa Ligi na kubwa zaidi wamedhamiria kuhakikisha pesa hiyo itatumiwa na vilabu katika kukidhi masuala ya usafiri ambao umekuwa changamoto kwa baadhi ya vilabu.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi amesema wao kama wadau wa michezo wamevutiwa na maendeleo ya Ligi Kuu ambayo imekuwa na ushawishi na kufanya vizuri katika viwango vya ubora barani Afrika.