Wednesday , 6th Oct , 2021

Shirikisho la mpira wa Miguu nchini TFF limesema bado halijapokea taarifa yoyote ya uthibitisho kutoka Shirikisho la mpira wa miguu Duniani FIFA iwapo kama wamewaruhusu washabiki kuingia katika mchezo wa kufuzu fainali za kombe la Dunia dhidi ya Benin utakaochezwa Oktoba 7, 2021.

Kikosi cha Taifa Stars wakiwa mazoezini

Akizungumza na East Africa Radio, Afisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo amesema kuwa hadi sasa hawajapata mrejesho kutoka FIFA ndio maana hawajatangaza viingilio kwa ajili ya washabikia ambao wangependa kushuhudia mchezo huo katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

''Mpaka sasa licha ya kufanya jitihada za kupata kibali cha kuruhusu washabiki kuingia uwanjani bado hatujapata jibu la moja kwa moja ndio maana unaona hatujatangaza viingilio vya mchezo wa kufuzu kombe la Dunia kati ya Taifa Stars dhidi ya Benin, Cliford Ndimbo Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa TFF akizungumza kupitia Kipenga.

Katika hatua nyingine Ndimbo amethibitisha kukamilika kwa maandalizi, huku imani kubwa ni kwamba Taifa Stars itafanya vizuri katika mechi hiyo ya kundi J.