Monday , 11th Oct , 2021

Timu ya Coastal Union ya Tanga kesho Jumanne ya Oktoba 12, 2021 itacheza mechi ya kirafiki mjini Mombasa nchini Kenya kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya NBC  Tanzania dhidi ya Maafande wa Ruvu Shooting.

Wachezaji wa Coastal Union wakipiga jeramba.

Coastal Union itajipima nguvu na Bandari FC katika Uwanja wa Tononoka mjini Mombasa.

Akizungumzia mchezo huo wa kirafiki Afisa Habari wa Coastal Union, Jonathan Tito amesema ni sehemu ya kujiweka sawa kabla ya kurejea kwa mechi za Ligi Kuu ya NBC Tanzania.

"Kipindi hiki cha kupisha mechi za timu za taifa vijana wetu walipewa mapumziko ya siku tano, hivyo baada ya kurejea mazoezini tumeona tujiweke sawa dhidi ya majirani zetu Bandari FC kabla ya kuwavaa Ruvu Shooting," alisema Tito.

Coastal Union itaendelea na mzunguko wa tatu wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Ruvu Shooting mchezo utakaopigwa Jumapili hii ya Oktoba 17, 2021 kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.

Tito amesema mchezo huo dhidi ya Ruvu ni muhimu sana kwao kwa kuwa katika michezo yao miwili ya mwanzo wametoka sare yote wakiwa nyumbani.