Saturday , 16th Oct , 2021

Patashika ya Ligi Kuu Tanzania bara, michezo miwili imeungurumishwa kunako viwanja viwili tofauti na matokeo ya michezo hiyo kila timu imeondoka na alama moja.

Makocha wa Mtibwa Sugar, Josph Omog(Kushoto) na Awadh Juma(Kulia) wakielekezana jambo mazoezini

Kwenye dimba la Kaitaba, wakatamiwa wa Kagera Sugar''wanankurukumbi'' wamejikuta wakiendelea kuusaka ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu kufuatia jioni ya leo kung'ang'aniwa na ''wana komakumwanya'', Mbeya City walipotoka suluhu.

Matokeo hayo yanawafanya vijana wa kocha Francis Baraza kuwa na alama mbili katika michezo mitatu waliyocheza wakiwa wamepoteza mmoja na sare mbili.

Vijana wa kocha Mathias Lule, Mbeya City wamejikita katika nafasi ya tatu katika msimamo wakiwa na alaa 5 katika michezo mitatu waliyocheza, wakishinda mmmoja na sare mbili.

Geita Gold wakiwa nyumbani wamelazimishwa sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Mtibwa Sugar na sasa wamepata alama yao ya kwanza katika historia yao kwenye Ligi Kuu Tanzania bara.

Sare hiyo inamaanisha Mtibwa, bado wanasotea ushindi wao wa kwanza katika Ligi Kuu, kwani wamepoteza mchezo mmoja huku wakiambulia sare mara mbili.

Kikosi cha kocha Ettiene Ndayiragije kipo mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu wakiwa nafasi ya 16 na alama moja wakati Mtibwa wapo nafasi ya 11 kwa alama zao mbili walizozikusanya.

Katika mchezo huo, Mtibwa walipoteza penati kupitia mkwaju wa Boban Zirintusa kuokolewa na mlinda mlango wa Geita Gold.

 

Bao la Geita lilifungwa na Dany Lyanga dakika ya 47 wakati lile la Mtibwa Sugar lilifungwa na Boban Zirintusa dakika ya 64 ya mchezo.

 

Kesho majira ya saa 8 mchana kitapigwa kati ya Mbeya kwanza ambao watakuwa wenyeji wa Dodoma Jiji katika dimba la Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya, wakati saa 10 Jioni, Coastal Union watakuwa wageni wa Ruvu Shooting.