Tuesday , 26th Oct , 2021

Mwanasheria wa Marehemu Diego Maradona, Matias Morla amekiri chanzo cha kifo cha mteja wake ni kutopata  huduma nzuri za kimatibabu pindi alipokuwa mgonjwa .

Gwiji wa soka wa Argentina, Diego Maradona akiwa ameshikilia kombe la Dunia la mwaka 1986 na Mwanasheria wa nyota huyo, Matias Morlaa (kwenye pciha ndogo)

Morla amesema “walimpa huduma  mbovu, ndio maana akafariki.nilimueleza kila mtu kuhusu hali ya diego na nikagundua  kwamba mwili wake umedhoofu  kutokana na kupungua kwa kiasi kikubwa cha maji”.

Maelezo hayo ameyatoa mbele ya ofisi ya mwendesha mashtaka mjini San Isidro,Argentina ambayo inachunguza kifo cha gwiji huyo ambaye alikuwa anapewa huduma chini ya uangalizi wa madaktari saba kuangalia afya yake.

Matias Morla amekwenda mbali zaidi na kuilalamikia familia ya Maradona kwa kitendo cha kutaka baba yao akatibiwe nyumbani kuliko kubaki hospitali kama madaktari walivyoshauri huku lawama zaidi akiwatupia mabinti wa Diego, Dalma and Gianinna kwa kumtenga kumuuguza baba yao.

Maradona 60, alifariki mnamo November 25 mwaka 2020 akiwa anaendelea na  matibabu baada ya kufanyiwa oparesheni ya kichwa kutokana na kuwa na tatizo la kuganda kwa damu.

Mbali na tatizo la  kuganda kwa damu, Diego Armando Maradona  alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya figo na moyo kutokana na athari za kukithiri  kwa matumizi ya pombe na madawa ya kulevya enzi za uhai wake.