Friday , 29th Oct , 2021

Michezo ya kuwania kufuzu kucheza ligi ya klabu bingwa Afrika kwa mpira wa kikapu Afrika Basketball Africa league ‘BAL’ inataraji kuanza rasmi leo Oktoba 29, 2021 kwenye uwanja wa ‘Indoor’ uliopo ndani ya uwanja wa Mkapa.

(Mabingwa wa Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam 2020 na Mabingwa wa Ligi ya Mpira wa kikapu taifa 2021, timu ya Kurasini Heat wakiwa na rais wa Shirikisho la Kikapu Tanzania, Phares Magesa.)

Michuano hiyo itaanza kwa michezo miwili ya ufunguzi, ambapo timu ya New Star kutoka Burundi itacheza na Cobra Sport ya Sudan Kusini saa 11:00 Jioni wakati muwakilishi wa Tanzania, Kurasini Heat itacheza na Brave Hearts ya Kenya saa 2:00 usiku.

Akizungumza na kipindi cha Michezo cha KIPENGA cha EA Radio, Rais w Shirikisho la Mpira wa kikapu nchini, Phares Magesa amesema maandalizi ya michezo hiyo yamekamilika kwa asilimia mia na anawataka Wantanzania kuiunga mkono timu yao ya Kurasini Heat ili isonge mbele.

Kwa Upande mwengine, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo amewaondoa shaka wapenzi na watazamaji wa mchezo huo kuwa, mipango ya Usalama wilayani hapo imeimarishwa maradufu hivyo wajitokeze kwa wingi.

Michezo hiyo itakuwa ikichezwa miwili miwili hadi kilele chake Oktoba 31, 2021 Jumapili huku wenyeji Kurasini Heat watafunga dimba kwa kucheza na City Oilers kutoka nchini Uganda.

Ratiba kamili ya michezo hiyo ya kuwania kufuzu BAL ni kama ifuatavyo:

Ijumaa Oktoba 29, 2021

Saa 11:00 Jioni, New Star (Burundi) vs Cobra Sport (Sudan Kusini)

Saa 2:00 Usiku,  Bravehearts (Malawi) vs Kurasini Heats (Tanzania)

Jumamosi Oktoba 30, 2021

Saa 11;00 Jioni, Ulinzi Warriors (Kenya) vs New Star (Burundi)

Saa 2:00 Usiku, City Oilers (Uganda) vs Bravehearts (Malawi)

Jumapili Oktoba 31, 2021

Saa 11:00 Jioni, Cobra Sport (Sudan Kusini) vs Ulinzi Warriors (Kenya)

Saa 2:00 Usiku, Kurasini Heats (Tanzania) vs City Oilers (Uganda)