Sunday , 12th Dec , 2021

Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kutofurahishwa na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya kazi vinavyofanywa na baadhi ya askari polisi nchini hasa wakiwa katika mazingira ya kazi.

Rais Samia akihutubia kwenye hafla ya kufunga mafunzo ya maofisa wa Polisi, Kurasini

Amesema hayo katika hafla ya kufunga mafunzo ya maofisa wa Polisi katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi Kurasini, Dar es Salaam, ambapo ametaja tukio la askari aliyeonekana hadharani akiisifia pombe ya kienyeji aina ya Nipa huku akiwa katika sare za polisi.

"Nataka nisema moja nililoliona juzijuzi askari polisi yuko na sare kwenye watu anaisifia pombe haramu, sijui na yeye mwenyewe alikuwa tayari yule?", amesema Rais Samia.

"Kwenye video amesema "usiisema vibaya pombe", tena ameipa jina zuri tu anasema NIPA inajulikana Kimataifa msikamatekamate watu hapa hii siyo pombe haramu. Yuko kwenye sare tena na watu, angalau angefanya utani yuko na wenzake. Sijui kama IGP ulimuona na kama ulimuona yuko wapi", ameongeza.

Maafisa wa polisi waliohitimu kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo hicho, SACP Lazaro Mambosasa ni 748 ambapo kati yao maafisa wanawake ni 90.