
Kocha Mkuu wa Mtibwa Jospeh Marius Omog(Kushoto) akiteta na msaidizi wake Awadh Juma(Kulia) katika mazoezi ya kikosi chao.
Mabao ya wakatamiwa hao ambao kwa mara ya kwanza walikuwa wakiutumia uwanja wao wa Manungu baada ya kuufanyia marekebisho, wameibuka na ushindi huo baada ya kufanya majaribio katika michezo saba iliyopita bila ya mafanikio.
Mabao ya Mtibwa Sugar yalikwamishwa kambani na Steve Nzigamasabo kwa mkwaju wa penati dakika ya 13 kabla ya Said Ndemla kupachika la pili dakika ya 67 ya mchezo na kuwahakikishia wenyeji alama tatu muhimu za kwanza tangu kuanza kwa msimu wa 2021/2021.
Matokeo haya ni faraja kwa viongozi na Kocha Mkuu Jospeh Marius Omog ambaye ujio wake ulitarajiwa kuifanya Mtibwa kuwa moto wa kuotea mbali lakini mambo yakaenda kombo katika mechi saba zilizopita.
Mabingwa hao wa zamani sasa wamefikisha alama tano baada ya mechi nane walizocheza wakiwa wanaendelea kushika nafasi za chini wakiwa katika nafasi ya 15 kwa alama zao 5 walizokusanya sawa na Geita Gold ambayo inaburuza mkia katika jedwali la msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara.