Saturday , 25th Dec , 2021

Watu wanne wamepoteza maisha baada ya gari la mizigo walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka, Desemba 23 mwaka huu, majira ya saa 03:00 asubuhi, katika mteremko wa Kishoju, Kata ya Kihanga wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Awadhi Haji

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Awadhi Haji, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari amesema kuwa gari hilo la mizigo lenye namba za usajili T 654 DRW na Tela lake lenye namba za usajili T 638 ADD lilikuwa limepakia shehena ya magogo, likitokea wilayani Karagwe kwenda mkoani Shinyanga.

Ametaja majina ya waliopoteza maisha kuwa ni Said Twalibu (27) mkazi wa Igombero Mkinga mkoani Tanga, aliyekuwa dereva wa gari hilo, Mohamed Seif (31) mkazi wa Mkinga pia mkoani Tanga, Emmanuel Salu mfanyabiashara wa Kahama na Yasin Gowa mkazi wa Tarime Mkoa wa Mara.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva aliyeshindwa kuchukua tahadhari alipofika katika eneo ilipotokea ajali kutokana na eneo hilo kuwa na mteremko mkali na kona kali.