Kikosi cha Yanga kikishuka kwenye Ndege, uwanja wa Ndege jijini Mwanza leo mchana
Kikosi cha Yanga kiliondoka Dar es salaam leo asubuhi kwenda jijini Mwanza na majira ya mchana kilikuwa kimefika. Awali mchezo huu ulikuwa uchezwe mkoani Geita lakini ukaamishiwa jijini Mwanza katika uwanja wa ccm Kirumba.
Kuelekea mchezo huu wachezaji wawili wa kikosi cha timu ya wananchi Dikson Job na Feisal Salum ‘Fei Toto” wote watarejea kwenye kikosi baada ya kumaliza kutumikia adhabu zao. Job alifungiwa michezo 3 na kamati ya Usimamizi na uendeshaji wa Ligi kwa kosa la kumkanyanga Richardson Ng'odya wa Mbeya City, wakati Feisal alikuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano.
Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa katika dimba la Benjamini Mkapa Dar es salaam Okotoba 02, 2021 Yanga ilinyuka Geita bao 1-0, bao pekee la mchezo huo lilifungwa na Jesus Moloko. Timu ya wananchi ndio vinara wa Ligi Kuu wanaongoza wakiwa na alama 42 na hawajafungwa mchezo hata mmoja katika michezo 16 waliocheza mpaka sasa.
Na wenyeji wao Geita Gold wanaoongozwa na kocha Fred Felix Minziro maarufu Baba Isaya, kikosi hicho kipo nafasi ya 7 kikiwa na alama 21 na hawajafungwa mchezo hata mmoja kwenye michezo 5 ya mwisho wameshinda michezo 2 na sare michezo 3.





