Wednesday , 9th Mar , 2022

Mashindano ya tennis ya BNP Paribas Open 2022 yanazidi kushika kasi mjini California nchini Marekani huku nyota kutoka Serbia Novak Djokovic akijumuishwa kushiriki huku kipengele cha wanaoshiriki kuwa wamepata chanjo ya Uviko 19 kikiibua sintofahamu kwa nyota huyo.

(Nyota wa tennis Mserbia Novak Djokovic)

Djokovic ambaye ni bingwa mara 20 wa mataji ya grandslam bado hajaweka wazi kuhusu hali yake ya kiafya kama amechanja au bado huku taarifa kutoka kwa waandaji wa michuano hiyo wakisema bado wanafanya mazungumzo na kambi ya nyota huyo.

"Novak ni miongoni mwa wachezaji watakaoshiriki kwenye michuano hii ndio maana kajumuishwa kwenye ratiba ingawaje bado tunafanya mazungumzo na kambi yake kama ataweza kushiriki kwenye tukio letu na kama ataweza kupata kibali maalumu kutoka CDC kwa ajili ya kuingia nchini ".taarifa kutoka kwa waandaji wa michuano hiyo BNP Paribas Open imesema mapema leo jumatano.

Mwezi uliopita baada ya kushindwa kushiriki kwenye michuano ya wazi ya Australian 2022 ,Novak Djokovic alisema hawezi kulazimishwa kitu kuingia mwilini mwake pasi na yeye kutaka na yupo radhi kukosa mashindano makubwa kama kigezo kitakuwa ni chanjo ya Uviko 19.

Novak Djokovic ambaye amepangwa kuanza katika hatua ya pili ya michuano hiyo atakuwa anasubiri saa 48 zijazo kujua hatma yake ya kuingia Marekani au ajiondoe kwenye mashindano hayo ambapo nyota kama Daniil Medvedev, Stefanos Tsitsipas,Andy Murray na bingwa mtetezi Cameron Norrie wanashiriki kwenye michuano hiyo yatakayo malizika jumapili ya March 20,2022.