Thursday , 5th May , 2022

Hali imezidi kuwa mbaya kwa Philadelphia 76ers baada ya kupoteza mchezo wa pili wa nusu fainali kanda ya mashariki dhidi ya Miami Heats kwa kupoteza kwa alama 119-103 katika dimba la FTX Arena.

Mchezaji wa Miami Heats, Bam Adebayo (Kushoto) akijaribu kumhadaa James Harden wa Philadephia 76ers katika mchezo wa leo ulioisha kwa Heats kushinda kwa alama 119-103

76ers wanaendelea kumkosa Joel Embiid ambaye ndiye mfungaji bora msimu huu, katika muendelezo wa mechi za nusu fainali baada ya kuumia kwenye mchezo wa robo fainali dhidi ya Toronto Raptors.

Nyota wa Miami, Jimmy Butler alikuwa mwiba mchungu kwa upande wa Philadelphia baada ya kufunga vikapu 22, asisti 15 na ribaundi 6 huku Bam Adebayo akifunga vikapu 23.

Kwa upande wa 76ers, jitihada za Tyrese Maxey aliyefunga vikapu 34 pamoja na James Harden aliandika alama 20 hazikuweza kuzaa matunda mbele ya mabingwa wa mwaka 2012 na 2013 waliokuwa na ngome imara ya ulinzi.

Mchezo wa tatu unatarajiwa kuchezwa siku ya jumamosi katika dimba la Wells Fargo Center, mchezo ambao utawalazimu 76ers kushinda ili kujihakikishia nafasi ya kurudi kwenye ushindani wa michezo saba ya nusu fainali.