Thursday , 16th Jun , 2022

Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa kituo mahiri cha mafunzo kwa wakulima na usimamizi wa mazao baada ya mavuno mkoani Dodoma kupitia mradi wa kupambana na Sumukuvu (TANIPAC) chini ya Wizara ya Kilimo mradi ambao utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 18.3.

Ujenzi wa kituo cha mafunzo kwa wakulima

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde, ametembelea mradi wa ujenzi wa kituo hicho unaotekelezwa katika eneo la Mtanana, wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

"Rais Samia Suluhu Hassan ametuongezea bajeti ya kilimo kutoka bilioni 294 hadi kufikia bilioni 953 mwaka 2022/2023, ambapo tumeweka mkazo kwenye utafiti wa mbegu bora, kuimarisha huduma za ugani, kujenga miundombinu ya umwagiliaji, ujenzi wa maghala na upatikanaji wa masoko ya mazao, bado tunahitaji kuimarisha mifumo yetu ya usimamizi wa mazao baada ya mavuno,"amesema Mhe. Mavunde

Mradi wa ujenzi wa kituo hicho utajengwa sambamba na maghala na vihenge vya kisasa vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 19,000, kiwanda cha kusaga, soko, eneo la kukaushia, hostel na nyumba za watumishi kitasaidia kwa kiasi kikubwa katika mkakati wa Wizara kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno kufikia tarakimu moja (single digit)ifikapo mwaka 2030.