Thursday , 16th Jun , 2022

Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson, amesema kwamba taarifa iliyonayo Bunge kuhusu Loliondo na Ngorongoro ni ile ya serikali iliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, na kwamba Bunge haliwezi kutumika kujibu maneno ya mitandaoni.

Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson

Kauli hiyo ameitoa hii leo Juni 16, 2022, wakati wa mjadala wa hoja ya bajeti kuu ya serikali na kusema wabunge wengi wametaja maneno ya kwamba zipo chokochoko kutoka kwa majirani kuhusu masuala yanayoendelea Loliondo na Ngorongoro.

"Bunge taarifa iliyonayo ni ile aliyoitoa Waziri Mkuu, hiyo ndiyo taarifa ya serikali kuhusu jambo la Ngorongoro na Loliondo, kwa hivyo hizo taarifa zingine tushughulike nazo kwa kadiri zinavyojitokeza huko ambako zinajitokeza ili iwe rahisi hata hao watu kupata ujumbe kama tunafikiri wataupata," amesema Dkt. Tulia

Aidha ameongeza kuwa, "Wakati tukiendelea na mjadala wa hoja ya bajeti kuu haya maneno ya chokochoko nimeyasikia wabunge wameyasema sana, kwa sababu huu ni Muhimili wa Bunge na huko tunakosema chokochoko zimetoka zimekuja kwa njia ya mitandao sisi hatuwezi kujibu chokochoko za mitandao kwa kutumia Bunge,".