Friday , 17th Jun , 2022

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni, amewapandisha vyeo maofisa wawili wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha wanaofanya kazi katika kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia baada ya kutoa huduma bora kwa watalii.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni, akimpongeza mmoja wa Maafisa aliowapandisha cheo

Mhandisi Masauni amewataja aliowapandisha vyeo kuwa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Waziri Tenga ambaye amepandishwa cheo kuwa Mrakibu wa Polisi (SP) na Mkaguzi wa Polisi Insp Anthony Mwaihoba ambaye amepandishwa cheo kuwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP).

 "Leo asubuhi nimepokea barua toka Ubalozi wa Tanzania nchini Italia ambayo iliandikwa na watalii raia wa Italia waliofika nchini hivi karibuni kwa ajili ya shughuli za utalii" amesema Waziri Masauni.

Amefafanua kuwa, katika barua hiyo watalii hao wametoa shukrani na pongezi baada ya kuridhishwa na huduma bora waliyoipata kutokana na changamoto za kiusalama walizokua nazo ikiwemo utapeli ambapo maofisa hao walifanya juhudi kubwa za kudhibiti uhalifu huo.

"Askari  hao wamekua mfano bora wa kuigwa kwa kuitangaza nchi yetu vizuri Kimataifa hususani kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anautangaza utalii kupitia filamu ya The Royal Tour,"ameongeza Waziri Masauni.