Monday , 20th Jun , 2022

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla leo amefanya kikao kazi cha maelekezo na viongozi wa ngazi ya wilaya, kata na Mitaa wakiwemo Madiwani, Wenyeviti wa Mitaa na Watendaji wa Kata/ Mitaa na kuwapatia maelekezo matano ya kutekeleza.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla

Miongoni mwa maelekezo hayo ni pamoja na Usimamizi madhubuti wa Operesheni ya anuani za Makazi ambapo amesema kwa Mkoa huo ni lazima zoezi Hilo lifanyike kwa ukubwa kwakuwa Dar es salaam ndio uso wa Nchi.

Aidha RC Makalla amewapongeza Viongozi na Wananchi kwa ushirikiano mkubwa walioonyesha kufanikisha awamu ya kwanza na kufanya Mkoa Kuvuka lengo kwa Asilimia 104 ambapo ameelekeza awamu hii ya pili ya uwekaji Nguzo kwenye Barabara, Mitaa na Vibao kwenye Nyumba kufanyika kwa Kasi na ufanisi.

RC Makalla amewataka Watendaji hao kuhakikisha Ifikapo August 23 kila Mwananchi anahesabiwa kwenye zoezi la Sensa ya watu na Makazi ili kuwezesha Serikali kujua idadi ya Wananchi na kuweza kupanga Bajeti na namna ya kutoa huduma.

Katika kikao kazi hicho, RC Makalla amewapongeza Wenyeviti wa Mitaa kwa kufanikisha Operesheni tokomeza Panya road jambo lililopelekea Jiji kuwa shwari ambapo ameelekeza agenda ya Ulinzi na usalama kuwa agenda ya kudumu kwenye vikao na mikutano.
Hata hivyo RC Makalla ameendelea kusisitiza Watendaji hao kudhibiti suala la Ufanyaji Biashara holela kwenye maeneo yaliyokatazwa ambapo amesema Mtendaji atakaeonekana kulegalega kwenye usimamizi atakuwa anapoteza sifa ya kuongoza eneo alilopo.