Wednesday , 29th Jun , 2022

Mbunge wa Makete Festo Sanga, ameiuliza Ofisi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, vigezo vilivyotumika kuajiri watu waliohitimua mwaka 2021 na kuwacha wa 2015 licha ya kwamba wapo wengine waliokuwa wanajitolea kwenye ofisi za serikali.

Mbunge wa Makete Festo Sanga

Swali hilo ameliuza Bungeni hii leo Juni 29, 2022.

"Hivi karibuni serikali imetangaza ajira mpya na kuna wale waliohitimu miaka ya nyuma na waliokuwa wanajitolea lakini wamekosa ajira, ni mfumo upi umetumika kuajiri mtu wa mwaka 2021 ukamuacha wa mwaka 2015? ambaye alikuwa anategemea kupata ajira,"amehoji mbunge Sanga.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deo Ndejembi amesema kuwa, "Ajira hizi za ualimu na afya zinaratibiwa na TAMISEMI, Utumishi tumetoa vibali tu, nafahamu kuna vigezo vilivyowekwa na vilifuatwa na wale waliostahili kuajiriwa na serikali katika dirisha hili wameajiriwa, na hao wengine huenda wanajitolea au wanasubiri kupata ajira basi nafasi yao itakuja, serikali ya awamu hii inaendelea kutoa vibali vya ajira, na wao waendelee kujitolea na waziombe nafasi hizi,".