Thursday , 30th Jun , 2022

Waziri wa Fedha na Mipango Dokta Mwigulu Nchemba amepokea gawio la shilingi bilioni 36.1 linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay.

Makabidhiano hayo ya hundi kifani yalifanyika katika Ofisi za Wizara ya Fedha Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma yenye hisa ndani ya Benki ya CRDB na Menejementi ya Benki ya CRDB.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Fedha aliipongeza Benki hiyo kwa kutoa gawio kwa Serikali, Dkt. Nchemba aliipongeza Benki ya CRDB kwa kupata matokeo mazuri ya fedha mwaka 2021 ambayo yamepelekea kuongezeka kwa gawio kwa wanahisa ikiwamo Serikali.

“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki yetu ya CRDB inazidi kuimarika zaidi kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo Watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii, alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alisema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitakwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeianisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2022/2023. Kipekee kabisa niipongeze Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB kwa kazi nzuri mnayoifanya, aliongezea Dkt. Nchemba.

Aliipongeza Benki ya CRDB kwa matokeo mazuri ya fedha iliyopata katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2020 ambapo faida ya Benki imeongezeka kwa asilimia 111 kufikia shilingi bilioni 90 kutoka shilingi bilioni 43 zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2021. Mkiendelea na kasi hii mwakani tunategemea kupata gawio nono zaidi, alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alizitaka taasisi nyengine kuiga mfano wa Benki ya CRDB katika kuleta faida kwa Serikali na Wanahisa kutokana na Uwekezaji. Alizitaka Taasisi na Mashirika yote ambayo Serikali inahisa kuweka mikakati madhubuti itakayoleta tija, huku akiwataka viongozi wake kutjitathmini kiutendaji.

Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa taasisi za fedha katika maendeleo ya taifa, Dkt. Nchemba aliipongeza Benki ya CRDB kwa kupunguza riba katika mikopo ya kilimo na wafanyakazi. Kiwango cha riba cha tarakimu moja katika mikopo ya kilimo kufikia asilimia 9 kutoka asilimia 20 iliyokuwa ikitozwa hapo awali ni cha kihistoria, hongereni sana, alisema.

Aidha, aliipongeza Benki kwa kutenga fedha kwa ajili ya uwezeshaji kwa kundi la wajasiriamali nchini kwa ajili ya kuwasaidia kuondokana na changamoto zilizotokana na janga la UVIKO-19. Kwa upande wa sekta ya kilimo alibainisha mkataba ambao benki hiyo imeingia na Shirika la Umoja wa Mataifa la GCF kuwezesha kilimo cha kisasa kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi utasaidia kuleta mapinduzi makubwa katika sekta hiyo nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema kuwa gawio hilo ni sehemu ya faida ya shilingi bilioni 268.2 baada ya kodi ambayo Benki hiyo imeipata katika mwaka wa fedha 2021. Pia ameeleza kuwa Benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora ili kukidhi mahitaji ya wanahisa wake na wananchi kwa ujumla.