Wednesday , 20th Jul , 2022

Mahakama ya wilaya ya Arusha imemhukumu kifungo cha maisha Fadhil Sumayani (30 )kwa Kosa la kulawiti na kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka tisa wa darasa la tatu katika shule ya msingi Emawoi wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Fadhil Sumayani, aliyefungwa kifungo cha maisha jela

Hukumu hiyo imetokana na kesi  ya ulawiti na ubakaji namba 31 ya mwaka 2021, ambapo imetolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Arusha Gwantwa Mwankuga .

Inadaiwa kuwa mshatikwa huyo mnamo Mei 19 alifanya kitendo hicho akiwa anatimiza majukumu yake ya ulinzi katika jengo lililopo katika Kijiji cha Seile wilayani Arumeru wakati mtoto huyo alipokuwa ametumwa na mama yake kwenda dukani kununua mahitaji ya nyumbani .

Inaelezwa kuwa Mama wa mtoto huyo baada ya kuona mwanaye amechukua muda mrefu alianza kumtafuta bila mafanikio yoyote na majira ya saa 3:00 usiku akatoa taarifa kwa  mwenyekiti wa eneo hilo na kisha kwenda kuarifu katika kituo cha Polisi .

Kesi hiyo ilikuwa na mashahidi watano na kwa mujibu wa shahidi namba tatu ambaye ni muuzaji wa duka aliieleza mahakama kwamba, wakati akiwa barabarani alimkuta mtoto huyo akiwa analia na pindi alipomhoji alimweleza kutendewa kitendo hicho na mtu huyo .

Kwa upande wa vielelezo kutoka hospitaini vilivyowasilishwa mahakamani hapo vilieleza mtoto huyo alionekana ameingiliwa kimwili na kukutwa na michubuko.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi amesema kulingana na ushahidi wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo vyao mahakama imemtia hatiani mtu huyo kwa kosa la ubakaji miaka 30 na kifungo cha maisha kwa kosa la ulawiti.