
“Mheshimiwa Mrema atakumbukwa kama kiongozi mkuu wa Chama cha TLP kwa muda mrefu sana. Na akiwa katika siasa, aliisaidia Serikali kupata mwelekeo mzuri wa vyama vya siasa," amesema Waziri Mkuu.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Agosti 24, 2022) wakati akizungumza na mamia ya waombolezaji kwenye ibada ya kumuaga marehemu Mrema katika Parokia ya Mt. Augustino Kilimahewa, Salasala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Amesema salamu za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ziliwasilishwa asubuhi na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango.
"Sisi tuliopo hapa tuna mambo mawili makubwa ya kufanya ili kumuenzi ndugu yetu Mrema. Moja ni kuenzi yale yote aliyofanya kwa upande wa Serikali na upande wa siasa lakini pili, tuendelee kumuombea ili Mwenyezi Mungu aweze kuilaza roho yake mahali pema peponi," amesema.
Kuhusu mazishi yake yanayotarajiwa kufanyika kesho Alhamisi huko Kiraracha, Moshi, Waziri Mkuu amesema Serikali itawakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Hamad Masauni.