Friday , 26th Aug , 2022

Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama  barabarani limetoa muda wa siku sita kwa wamiliki na madereva wa vyombo vya moto vikiwemo magari, pikipiki zote za magurudumu matatu na trekta kuweka viakisi mwanga ili kukabiliana na ajali za barabarani

Maagizo hayo yametolewa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Mkuu wa Oparesheni Mkoa wa Mbeya, Abdi Issango wakati akimuwakilisha Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ulrich Matei kwenye ufunguzi wa mafunzo ya viakisi mwanga yaliyofanyika wilayani Mbarali.

Amesema Jeshi la Polisi limetoa elimu juu ya umuhimu wa vyombo vya moto kuwekwa viakisi mwanga  ili kukabiliana na ajali hususani nyakati za usiku na kwamba baada ya hapo oparesheni ya kuwakamata madereva wakaidi itaanza.

“Leo tumeanza  kutoa elimu kwa madereva wa maguta, trekta, bajaji na kosta lakini elimu hii ni kwa wote, tunatekeleza maagizo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camilius Wambura kwamba kila mkoa utoe elimu ya umuhimu wa viakisi mwanga,” amesema Issango.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Yusuph Kamota amesema miongoni mwa mikakati ya kupunguza ajali mkoani humo ni pamoja na kuwekwa viakisi mwanga kwenye vyombo vya moto.

Amesema wilaya ya Mbarali ni miongoni mwa maeneo yenye vyombo vingi vya usafiri ambapo kwa sasa kuna pawatila 3000 ambazo zinatumika kusafiri abiria na shughuli za kilimo.

“Tumetoa elimu kwa madereva  na kuwaonesha namna wanavyotakiwa kuweka viakisi mwanga kwenye vyombo vya moto   naamini kila mmiliki au dereva atatekeleza agizo hili kwa mujibu wa sheria barabarani,” amesema Kamota.

Aidha Kamota amepiga marufuku madereva wa maguta na pawatila wilayani Mbarali kuacha tabia ya kusafirisha abiria kwani vyombo hivyo ni maalum kwa ajili ya kusafirisha mizigo.

Helson Zabron mmiliki wa pawatila amesema elimu ya viakisi mwanga imekuja wakati muafaka na kwamba wako tayari kulitekeleza.