Sunday , 11th Sep , 2022

Waziri wa Habari Nape Nnauye, ametoa onyo kwa viongozi wa makundi ya WhatsApp (Admin), na wote wanaohusika kusambaza mitandaoni jumbe na video fupi zinazohamasisha vitendo vya usagaji na ushoga na kwamba msako wa kuwakamata utaanza.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye

Kauli hiyo ameitoa hii leo Septemba 11, 2022, wakati akizungumza kwenye ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Jijini Dar es Salaam na kusema mbali na wengine kutumia makundi ya WhatsApp wapo wanaotumia maudhui ya cartoon zinazopendwa na watoto kupandikiza ushoga na usagaji.

"Kabla ya kuanza msako huu maalum wa kuwakamata na kuwasomba wote wenye kutuma, kuzalisha na kusambaza maudhui haya ni vyema sasa Watanzania wakajiepusha kwenye hili," amesema Waziri Nape

Aidha Waziri Nape ameongeza, "licha ya watu wachache kujaribu kuvuruga lakini anga ya mawasiliano kwa Tanzania iko salama na hatutamvumilia yeyote atakayejaribu kuichafua,".