Friday , 16th Sep , 2022

Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imesema kuwa ili kupata matokeo mazuri ya elimu ni lazima kuhakikisha upatikanaji wa lishe bora shuleni ili kuwajengea wanafunzi afya bora na kupata utulivu wa akili wawapo madarasani.

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Omary Kipanga

Akizungumza  Jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya Utiaji Saini Fomu ya kujiunga na muungano wa chakula shuleni Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh.Omary Kipanga amesema kuwa Pamoja na kuwepo kwa sera hiyo, utoaji wa huduma ya chakula shuleni umekuwa ukitekelezwa katika shule kwa namna na viwango tofauti.

" Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inafafanua kuhusu upatikanaji wa huduma muhimu katika shule na vyuo ikiwemo huduma ya chakula bora, maji safi na salama na upatikanaji wa huduma za afya kwa wanafunzi ndio maana leo kwa pamoja hapa tunatia saini fomu ya kujiunga na Muunganowa ChakulaShuleni nia ni ile ile ya kuhakikisha wanafunzi wanasoma vizuri na kupata matokeo mazuri . "Amesema Mh. Omary Kipanga .

Aidha Kipanga amesema Mwezi Oktoba, 2021 Wizara ya Elimu ilizindua Mwongozo wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimu ya msingi ili kuweka utaratibu wa kitaifa ambao utawezesha wanafunzi kupata huduma hiyo muhimu.

"Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakinufaika na wengine kukosa huduma hiyo muhimu sasa naamini kupitia Muungano huu utasaidia kuziba yale mapengo yaliyokuwepo na wanafunzi sasa hawatakuwa na sababu yeyote ya kutopata matokeo mazuri," Amesema Omary Kipanga.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Sarah Gordon-Gibson amesema kuwa moja ya njia ya kufikia malengo kwa taifa lolote duniani ni lazima kuwekeza kwa watoto hivyo ili kufikia huko lishe ni eneo linalohitaji maboresho makubwa huku Mkuu wa Ofisi Ndogo ya Shirika la Mpango Chakula Duniani (WFP) Dodoma  Nima  Sitta amesema ni muungano wa kimataifa wa chakula shuleni ni jukwaa la kuhakikisha nchi zote duniani ifikapo 2030 kila mtoto anapata angalau mlo mmoja shuleni.

Nao baadhi ya wanafunzi wakiwemo Beatrice Mtembi wa shule ya Sekondary Dodoma na  Lucas Mathias anayesoma shule ya msingi ya mfano Chifu Mazengo wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo muhimu kwani itasaidia kuongeza ufaulu darasani na kuepuka vishawishi vitakavyosababisha kutotimiza ndoto zao.