Thursday , 29th Sep , 2022

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana, amezindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) jijini Arusha. 

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana, akipeana mkono na Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema serikali chini ya Rais wa jamhuri ya Muungano wa TanzaniaaSamia Suluhu Hassan, ina imani kubwa na bodi hiyo katika kuleta maendeleo ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorogoro na sekta ya utalii kwa ujumla.

Amesema anataraji kuona Bodi hiyo  yenye wajumbe wenye elimu za juu na uzoefu mkubwa chini ya Mwenyekiti Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo, itabuni vyanzo vipya vya utalii ili kwenda na kasi ya matokeo chanya ya kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya The Royal Tour.

"Ni vizuri Bodi mkajikita katika kuboresha mifumo ya uendeshaji wa shirika kutoka uhifadhi wa asili mpaka uhifadhi wa kibiashara, kuendesha shirika kibiashara kutaifanya taasisi hii iingize watalii wengi na hivyo kuongeza mapato kwa nchi kutokana kuwepo kwa maboresho makubwa" amesema Waziri Chana.

Awali  akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Ndugu Juma Mkomi ameithibitishia Bodi hiyo kuwa Wizara itaendelea kutoa ushirikiano ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa.