Friday , 7th Oct , 2022

Klabu ya Tanzania Prisons na Singida Big Stars zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, zimepigwa rungu la kutofanya usajili kwa kipindi cha dirisha moja huku makipa Mussa Mbissa na Metacha Mnata wakiwa chanzo.

kikosi cha Singida Big Stars

Taarifa ya kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu iliyotoka leo Oktoba 7, 2022 imeeleza timu hizo zimefungiwa kutokana na kufanya usajili wa wachezaji hao ilihali wakiwa na mikataba na klabu zao za awali.

Taarifa hiyo imeeleza, Singida ilimsajili Metacha huku akiwa bado na mkataba na Polisi Tanzania hivyo hivyo kwa Prisons iloyomsajili Mbisa huku akiwa bado na mkataba na Coastal Union.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, uamuzi huo umezingatia kanuni ya 47 (21) ya Ligi Kuu na hata hivyo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imezikumbusha klabu zote nchini kuwa ussjili wa wachezaji unafanywa kwa kuzingatia kanuni na timu ambazo zitakiuka kanuni hizo, zitachukuliwa hatua.