Monday , 10th Oct , 2022

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema anatarajia kuiwakilisha Serikali ya Tanzania katika Kikao cha 73 cha Kamati Tendaji ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wakimbizi (UNHCR).

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni

Kikao hicho ambacho kinaanza leo Jumatatu Oktoba 10, 2022, kitafanyika katika jijini la Geneva, nchini Uswisi, Ulaya Magharibi kitajadili masuala mbalimbali yakiwemo jinsi ya kuwahifadhi na kuwasimamia Wakimbizi waliopo katika nchi mbalimbali duniani.

Waziri Masauni ameambatana na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Wakimbizi wa Wizara hiyo, Sudi Mwakibasi tayari wamewasili jijini Geneva nchini hapa, Jumapili Oktoba 9, 2022, akiwa tayari kuiwakilishi Tanzania katika Kikao hicho kwa kutoa taarifa ya Wakimbizi waliopo nchini.

Masauni na wasaidizi wake wamepokelewa na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania nchini Uswisi, Maimuna Tarishi, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu Tanzania, Hoyce Temu na Maafisa mbalimbali wa Ubalozi huo na baadaye kufanya kikao na maafisa hao wa ubalozi.

Akizungumza katika kikao hicho cha mapokezi kilichofanyika ofisi za ubalozi huo, jijini humo, amemshukuru Balozi Tarishi pamoja na maafisa wake kwa mapokezi mazuri na ameomba ushirikiano nao zaidi mpaka kikao hicho cha siku tano kitapomalizika.

“Mheshimiwa Balozi pamoja na maafisa wote wa ubalozi huu, nawashukuru sana kwa mapokezi mlionipa, nashukuru kwa miongozo mbalimbali kuhusu kikao hicho, naamini tutakuwa pamoja katika kuiwakilisha Serikali katika siku zote za kikao,” alisema Masauni.