Friday , 28th Oct , 2022

Askofu mkuu wa makanisa ya AICT nchini Mussa Magwesela  amewataka viongozi wa Dini nchini kutumia nyumba za Ibada kutoa Elimu ya kujikinga na maambukizi ya homa ya kirusi cha Ebola, ili utakapoingia nchini kila mtu aweze kujikinga.

Magwesela ameyasema hayo wakati anafungua mafunzo ya Elimu ya kujikinga na homa ya Ebola kwa viongozi wa Dini mkoani Geita na kuwasisitiza kuitoa Elimu hiyo kwa usahihi ili wananchi waweze kuchukua tahadhari. 

"Hizi Elimu ambazo tunazipata tuhakikishe basi ni zile ambazo zinaweza zikawasaidia Watanzania wenzetu ambao tunakutana na wao katika Misikiti tunakutana na wao katika nyumba za Ibada katika Makanisa yetu tunawaongoza, tunawasaidia na kwa sababu hiyo basi niwasisitize sana na kuwahamasisha sisi sote tuweze kushirikiana kwa pamoja", alisema Magwesela.

Kwa upande wake mkurugenzi wa program za maendeleo na utetezi CCT, Clotilda Ndezi anaelezea lengo la kutoa Elimu hiyo kwa viongozi wa Dini huku mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Paschazia Maduku akielezea mipango ya kimkoa dhidi ya Ugonjwa wa Ebola.

"Kwa sababu mkisema ninakumbuka hata Rais wetu mama Samia alisema kwamba, viongozi wa Dini mkisema yale maneno yenu, yanaingia yani kwenye Roho kwenye Moyo, lakini maneno mengine yakisemwa yanaingia tu kwenye akili, kwahiyo ya kwenu yana nguvu kwa sababu  yanagonga kabisa kwenye Moyo na kuleta mabadiliko ya mtazamo", anesema Ndezi

"Tuna mkakati wa kuweza kufikia makundi mengine kwa mfano kundi la wazee tupo tunafanya maandalizi, pia tunategemea kuwafikia viongozi wa makundi ya walemavu walioko katika mkoa wa Geita, watatusaidia nao kuwafikia pia kuwafikishia kwa sababu wale watu pengine inaweza ikawa ngumu kupata Elimu hii lakini kupitia viongozi wao wanaweza wakapata hii Elimu", amesema Madulu