Monday , 31st Oct , 2022

Wananchi wa Kijiji cha Bugando, Kata ya Nzera, wilayani Geita mkoani humo, wameiomba serikali ichunguze na kumtafuta mtu anayewaingilia usiku wananchi kwenye nyumba zao na kuwabaka hali inayopelekea kuishi kwa mashaka na kuhataraisha afya zao.

Mmoja wa wanawake walioingiliwa kishirikina

Wakizungunza na EATV waathirika wa tukio hilo wanasema mtu huyo amekuwa akiingia kwenye nyumba zao na kuwaingilia kimwili kwa nguvu na badae anaondoka bila kuchukua kitu chochote kwenye nyumba zao. 

"Yani anakuja kwa mazingira ya kawaida anaingia tu yeye mwenyewe sikumuona sura aliponanilia akawa ameiwasha simu yake alipoiwasha simu akanambia usinitazame, nikamwambia sasa wewe nani, akanambia haupaswi kujua, kwanza akaniuliza una watoto, badae alipomaliza kunaniliu hivyo akawa ameondoka, kwakweli sikubahatisha hata kumuona, ndio hivyo akawa amenibaka," amesema mmoja wa waliobakwa kishirikina

Diwani wa Viti Maalum wa Kata hiyo Victoria Ndaki, amesema wameanza kufanya vikao kwa ajili ya kuwatambua wanaofanya vitendo hivyo japo Jeshi limezuia kutokana na sababu za kiusalama.

Mkuu wa wilaya ya Geita Wilson Shimo ameiagiza serikali ya Kata kwa kushirikiana na serikali kuu kuanza uchunguzi ili kuweza kuwabaini watu wanaofanya vitendo hivyo.

"Nimeona akina mama hao na kuongea na viongozi wa hapa Nzera na wameshuhudia kwamba haya matendo yanaendelea hapahapa Nzera, vitendo ambavyo sio vya kiungwana na si vya kiutu, tunaanza kufuatilia kwa ukaribu zaidi mienendo na tabia ya watu wanaofanya vitendo hivyo," amesema DC Shimo.