Friday , 4th Nov , 2022

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeitikia wito wa Bunge uliotolewa na Spika wa Bunge wa kuwataka wafike kwenye Kamati ya Kudumu ya Huduma za Maendeleo ya Jamii ili kujieleza kwanini hawataki kusikiliza maelekezo ya Serikali katika utoaji wa mikopo

Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badruk, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu Prof. Khamis Dihenga na baadhi ya wajumbe kutoka HESLB

Akiongea mara baada ya kutoka kwenye kikao hicho msemaji wa bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu HESLB Omega Ngole amesema walipata wito wakuitwa Bungeni na  kamati hiyo ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii na wameitikia wito lakini ni mapema sana kuongelea kile kilichoongelewa kwenye kikao hicho kwani bado wapo kwenye vikao ambavyo vimeanza leo.

Spika wa Bunge, Dk Tulia alitoa agizo hilo Bungeni baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda na baadhi ya wabunge kulalamikia kuwa kamati aliyoiunda na (Profesa Mkenda), kuchunguza utoaji wa mikopo ya elimu ya juu imeshindwa kupata ushirikiano.

Bunge liliazimia wanafunzi wote wenye vigezo vya kupata mikopo na hawajapata mikopo mpaka sasa, serikali iangalie utaratibu mzuri wa kuwawezesha wanafunzi hawa kupokelewa vyuoni ili waendelee na masomo yao wakati serikali ikitafuta fedha kwa ajili ya mikopo.