Sunday , 6th Nov , 2022

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila, amesema ndege ya Precision Air iliyoanguka leo asubuhi ndani ya Ziwa Victoria Bukoba Kagera, ilikuwa na jumla ya watu 43.

Zoezi la uokoaji likiendelea

Akiongea na waandishi wa habari eneo la tukio, Chalamila amesema zoezi la uokozi linaendelea na tayari watu 26 wameshaokolewa.

''Ndege ilikuwa na jumla ya watu 43. Kati yao 39 ni abiria, wawili ni wahudumu na wawili ni marubani. Tumefanikiwa kuokoa watu 26 wamepelekwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kagera. Tunaendelea na uokozi kwa kuivuta ndege. Mpaka sasa bado tuna mawasiliano na marubani'' - Amesema Albert Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Aidha Mkuu huyo wa mkoa wa Kagera ameibanisha ndege hiyo ya kampuni ya Precision Air kuwa ni ATR 42 yenye namba za usajili 5XPWF, ilikuwa ikitokea Dar es Salaam na imeanguka majira ya saa 2:20 asubuhi.

Ameeleza kuwa tayari wameshamjulisha Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa juu ya ajali hiyo huku pia wakipokea salamu za pole kutoka kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.