Monday , 7th Nov , 2022

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha usafiri wa anga unakuwa salama na unazingatia viwango vinavyohitajika kitaifa na kimataifa

Akizungumza wakati wa zoezi la kuaga miili 19 ya watu waliopoteza maisha katika ajili ya ndege iliyotokea jana kwa kutumbukia katika ziwa Victoria mita 500 kufikia mwanzo wa barabara ya kutua ndege, Waziri Mkuu huyo amesema kuwa usafiri wa anga ni salama.

"Niwatoe hofu Watanzania waendelee kutumia usafiri wa anga kwa kuwa mamlaka zote husika zipo na zinaendelea kuchukua hatua sitahiki ya kuhakikisha unakuwepo usalama wa anga kwa ajili ya safari za ndani ya nchi" amesema.

Aidha akitoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, waziri mkuu huyo amesema kuwa Rais ameelekeza kwamba mazishi ya waanga wote wa ajali hiyo yatagharamiwa na serikali.

Kwa upande wake waziri wa ujenzi na uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa taarifa zinaonyesha kuwa muda wa saa mbili kamili asubuhi Bukoba hali ya hewa ilikuwa nzuri, lakini ilibadilika ghafla wakati rubani akikaribia kutua na kusababisha ajali hiyo.

Jana Novemba 06 majira ya asubuhi ndege ya shirika la Precision Air ikitokea Dar-es-salaam kuelekea Bukoba kupitia mkoa wa Mwanza, ilipata ajali na kutumbukia katika ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 19 huku watu wengine 26 wakiwamo 24 waliokuwa wasafiri katika ndege hiyo wakiokolewa.