Monday , 7th Nov , 2022

Wizara ya masuala ya kidini ya nchini  Somalia imepiga marufuku matumizi ya jina al-Shabab  ikitafsiriwa "vijana" kwa Kiarabu  na kuwataka wananchi kulitaja kundi hilo la wanamgambo kama "Khawarij", neno la dharau linalomaanisha dhehebu lililopotoka

.

  Katika taarifa, wizara hiyo pia ilipiga marufuku masheikh kushughulika na wanamgambo washirika wa al-Qaeda au kukutana nao.

Serikali imesema agizo la kuitaja al-Shabab kama "Khawarij" ni sehemu ya vita dhidi ya kundi hilo.

Hii si mara ya kwanza kwa serikali ya Somalia kubuni jina jingine la al-Shabab.

Mwaka 2015 serikali iliviambia vyombo vya habari kulitaja kundi hilo la wanamgambo kama "Ugus", kifupi cha Somalia cha "kikundi kinachowaua watu wa Somalia".

 Kundi hilo la  al-Shabab likajibu mapigo kwa kutishia kumuadhibu mtu yeyote, wakiwemo waandishi wa habari, ambao walitii maagizo ya serikali au kutumia neno hilo.

Mwezi uliopita, mamlaka ya shirikisho ilipiga marufuku vyombo vya habari vya ndani kuripoti kuhusu shughuli za al-Shabab.