Tuesday , 8th Nov , 2022

Maafisa Maendeleo ya Jamii wametakiwa kujipanga kwenda na kasi ya serikali ili kuchochea maendeleo ya jamii sambamba na sera, mikakati, sheria  na miongozo mbalimbali wakati serikali ikiendelea kufanyia kazi changamoto za upungufu wa watumishi, mazingira ya kazi na sheria ya taaluma hiyo.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Dk. Dorothy Gwajima

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ameyasema hayo akifungua kikao kazi cha maafisa hao wa sekretarieti za mikoa na wakuu wa idara za maendeleo ya jamii wa mamlaka za serikali za mitaa jijini Dodoma Novemba 08, 2022 alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa kada hiyo.

Dkt. Gwajima amesema, serikali ina matumaini makubwa na mchango wa kada hii na itahakikisha inafanya uwezeshaji ili kwenda na kasi iliyokusudiwa. 

"Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan anatambua umuhimu wa sekta ya Maendeleo ya Jamii katika kuiwezesha Jamii kushiriki kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali walizonazo hivyo kuwa kitovu cha maendeleo" na ndiyo maana amechukua hatua ya kuunda wizara mama ya sekta hii na mambo mengi mazuri yanakuja" Amesema Waziri Dkt. Dorothy Gwajima.

Akielezea umuhimu wa kada ya maendeleo ya jamii kwenye sekta zote amewapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuwezesha mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto huku akirejea mpango kazi wa Taifa wa kupambana na ukatili huo kwamba serikali inakamilisha ya utekelezaji wa miaka mitano iliyopita ili kuja na mpango mpya ambao utajibu mahitaji ya sasa kwenye mapambano haya.