Friday , 18th Nov , 2022

Katika kukuza diplomasia na uchumi, Afrika Kusini na Tanzania zitashirikiana katika kazi za utamaduni na utalii, huku wananchi wakihimizwa kutumia kazi za utamaduni kukuza uchumi wa mataifa haya mawili na kuonywa kudharau utamaduni wa Afrika.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo  Yakub Said

Akizungumza na Wanahabari Leo Novemba 18,2022 Jijini Dar es salaam Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo  Yakub Said  amesema Nchi  ya Afrika Kusini  imefungua rasmi Msimu wa  Utamaduni wa Afrika kusini nchini Tanzania kutokana na kutambua mchango mkubwa wa Tanzania katika  ukombozi wa nchi yao.

Aidha Yakub ameeleza kuwa Afrika Kusini imeamua kufanya shughuli mbalimbali za utamaduni na utalii katika kipindi cha msimu huo, kutoka na ushirikiano mkubwa baina ya mataifa haya. 

Kwa upande wake Mnata Resani ambaye ni Mkurugenzi wa Lugha Wizara ya Utamaduni, amebainisha kuwa hii ni fursa ya kuendelea kukuza lugha ya Kiswahili kwenye mataifa mengine.

Hata hivyo ameeleza kuwa Msimu huo utaenda sambamba na Maonyesho,Semina pamoja na utalii wa Maeneo mbalimbali yenye historia ya kumbukumbu ya nchi ya Afrika kusini.

Msimu huo umefunguliwa rasmi leo Novemba 18 na kutarajiwa kumalizika Desemba 04,2022 kwa kushiriki kwenye burudani mbalimbali likiwemo tamasha la wiki ya ubunifu wa mavazi.