Tuesday , 29th Nov , 2022

Afisa mazingira na utalii wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Peter John, amesema kwamba mtu yeyote atakayekamatwa akijisaidia haja ndogo ama kubwa katika fukwe ya bahari au fukwe ya soko la samaki Feri, atatozwa faini ya shilingi laki tatu kwa kila kosa.

Wavuvi wakiendelea na shughuli zao katika ufukwe wa Feri jijini Dar es Salaam

Hatua hiyo imekua baada ya wavuvi katika soko la Feri kuiomba serikali kuinusuru fukwe hiyo kwa kuweka sheria kali kufuatia baadhi ya watu kujisaidia haja ndogo na hata kubwa kwenye eneo hilo.

Wakizungumza leo Novemba 29, 2022, na EATV wavuvi hao wamesema suala la mtu kujisaidia haja ndogo na kubwa katika fukwe hiyo limeonekana kama ni la kawaida hivyo serikali inapaswa kulipa uzito bila kusubiri mpaka kutokeaa madhara ya kiafya ikiwemo magonjwa ya milipuko.