Thursday , 8th Dec , 2022

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itaendelea kuongeza nguvu katika jitihada za Kuzuia na Kupambana na ujangili wa wanyamapori na Biashara ya nyara na mazao ya misitu ili kutokomeza kabisa vitendo hivyo vinavyoathiri taswira ya nchi, uchumi na maendeleo ya uhifadhi

Hayo yamebainishwa leo jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo Wenyeviti wa Kamati za Kanda za Kiikolojia za Kuratibu Doria (TCG's) katika kukabiliana na ujangili na Biashara haramu ya wanyamapori nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Msaidizi wa Uzuiaji Ujangili na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi Taifa cha Kuzuia na Kupambana na Ujangili nchini Bw. Robert Mande , Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. John Ngowi amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mafunzo na doria ili kuhakikisha majangili wanaokamatwa wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Amesema mkakati uliopo katika mapambano dhidi ya ujangili ni kuona watuhumiwa wote wanaokamatwa wanafikishwa mahakamani na mashauri yao yanaendeshwa haraka na kwa ufanisi ili adhabu inayostahili iweze kutolewa kulingana na matakwa ya sheria.

“Lengo la kutolewa kwa mafunzo haya ni kuharakisha na kuhakikisha majangili wote wanaokamatwa wanafikishwa mahakamani na mashauri yao yanaendeshwa kwa haraka na kwa ufanisi ili wahusika wapewe adhabu inayostahili kulingana na matakwa ya sheria za nchi yetu” Amesisitiza.

Amesema ujangili unaathiri ustawi wa jamii na kudumaza uchumi wa nchi hivyo  mafunzo hayo yatawasaidia Wenyeviti hao kupanga mikakati endelevu ya kukabiliana na ujangili huku akibainisha kuwa mitandao ya uhalifu wa rasilimali hizo wakati mwingine huanzia nje ya nchi ikihusisha watu wengi katika ngazi mbalimbali na inafadhiliwa na watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha.

'' Ni imani yangu kuwa baada ya mafunzo haya wananchi wataanza kuona majangili wanachukuliwa hatua kali za kisheria zinazostahili.  Wataanza kuogopa kushiriki katika  vitendo vya ujangili'' Amesema Afisa Wanyamapori Mkuu, Ngowi

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia Watendaji wa Idara na Taasisi zinazohusika na ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori na mazao ya misitu kupanga mikakati endelevu ya kukabiliana na ujangili hapa nchini pamoja na kuimarisha dhana ya umoja inayowezesha Idara na Taasisi za ulinzi wa wanyamapori na misitu kufanya kazi kwa pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Kupambana na Ujangili na Usafirshaji haramu wa Nyara, Theotimos Rwegasira amesema mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo Duniani (UNDP) na Shirika la Mazingira (GEF) yatasaidia kupunguza ujangili kwa kiwango kikubwa.

 Amesema mafunzo hayo yatakayohitimishwa leo yanatarajiwa kuleta mafanikio makubwa katika vita dhidi ya ujangili ikiwa ni mwendelezo kuunga juhudi mkono juhudi za serikali za kukabiliana na ujangili.