Monday , 12th Dec , 2022

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepewa tuzo ya kimataifa ijulikanayo kama International Iconic Awards ya nchini India kwa kutambua mchango wake katika kuasisi na kushiriki kwa umahiri mkubwa katika programu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imekua na matokeo chanya kwa jamii inayomzunguka.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, akiwa ameshika tuzo alizopewa Rais Dkt.Samia

Tuzo hiyo imekabidhiwa jijini Dodoma na Uongozi wa Miss Jungle International na Bega kwa Bega na Mama (BBMF) kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, ili aweze kuifikisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.  Samia Suluhu Hassan.

Akipokea tuzo hizo, Waziri Balozi Dkt. Chana amesema Dkt. Samia, ametoa mchango mkubwa katika kuinua sekta ya utalii nchini hasa baada ya athari kubwa ya janga la UVIKO 19 akiongeza kuwa filamu ya Tanzania The Royal Tour imesaidia kutangaza vivutio vya utalii na kuvutia watalii wengi nchini.

Aidha Waziri Balozi Dkt. Chana, ametoa wito kwa wadau wa utalii waendelee kutekeleza kwa vitendo malengo ya Tanzania – the Royal Tour ili kuweza kufikia azma iliyokusudiwa katika kukuza na kuendeleza sekta ya utalii nchini na kushukuru Miss Jungle International ambao walipokea tuzo husika na kuja kuikabidhi kwa Rais.