Monday , 12th Dec , 2022

Takriban watu 40,000 wameyakimbia makazi yao kufuatia mapigano mapya katika jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Upper Nile nchini Sudan Kusini, shirika la Umoja wa Mataifa limesema.

Katika taarifa yake ya hivi karibuni, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (Ocha) ilisema vitisho vya ghasia vinaendelea kutatiza  maisha ya wananchi  katika jimbo hilo.

Taarifa Ilisema watu waliokimbia makazi yao wanaishi katika mazingira mabaya na wanahitaji msaada wa haraka wa kuokoa maisha.

Wiki iliyopita waangalizi wa kusitisha mapigano walisema watatuma timu kuchunguza mapigano yanayoendelea kushuhudiwa katika jimbo hilo.

Mapigano yameripotiwa katika jimbo hilo tangu katikati ya mwezi Novemba - yakiripotiwa kuhusisha jeshi la taifa na vikosi vya upinzani vya Maiwut.

Pia kuna ripoti za uhasama mpya katika eneo la Fashoda kati ya makundi tofauti hasimu ya kikabila.