
Akizungumza na wanahabari waliofika kujionea uendeshwaji wa Bandari ya kwanza kihistoria kujengwa katika nchi za Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki, Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Athuman Mrisha amesema Bandari hiyo ilianza miaka ya 1914 huku gati ya kwanza na ya pili ikijengwa mwaka 1954 na ukarabati wake wa kuipanua ili meli kubwa ziweze kutia nanga kwa wingi na kwa wakati mmoja ulianza mwaka 2019 kwa Hayati Rais Dk.John Pombe magufuli kutoa fedha za ujenzi
Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameendelea kutoa fedha za kukamilisha ujenzi huo mkubwa ambapo kidunia kwa sasa sekta ya usafirishaji mizigo kwa njia ya majini umeongezeka na unatumia gharama ndogo ikilinganishwa na zamani huku ukiongeza pato la taifa.
Katika hatua nyingine Mrisha amesema gharama zinazotumika kuboresha Bandari hiyo ni zaidi ya shilingi Bilioni 429 mpaka kukamilika kwake na unategemea kuhudumia tani milioni tatu kwa mwaka kwani kwa sasa wanahudumia tani laki 7 na nusu kwa mwaka
Madereva wa magari makubwa ya mizigo wanaofika kupakua na kupakia mizigo pamoja na wateja wa Bandari hiyo wamewataka wenzao kutoharibu miundombinu hiyo ya bandari ili kodi za watanzania zilizotumika kujengea zirudishe faida kwa wananchi kupitia kodi zinazolipwa na wafanyabiashara wa mizigo huku Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga akisema upanuzi wa Bandari ya Tanga imetengeneza ajira na kuongeza pato la taifa
Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Pili Mnyema amesema mradi huo unatarajia kukamika mwezi Aprili mwaka 2023 kama hakutakua na changamoto yoyote katika ujenzi huo.