Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris
Kwenye ziara hiyo ya kwanza nchini Tanzania na barani Afrika, anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia, ambapo pamoja na ujumbe wake pia watatembelea Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam na kukutana na vijana wajasiriamali wa Tanzania.
Pamoja na mambo mengine, ziara hiiyo ya Makamu wa Rais inalenga kuongeza nguvu katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania hususan baada ya kufanyika kwa mkutano kati ya Marekani na nchi za Afrika maarufu kama US - Africa Summit mwezi Desemba 2022, ambapo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alihudhuria.
Ziara hii inafanyika takribani miezi 11 tangu viongozi hawa wawili wanawake walipokutana Ikulu ya Marekani na kubadilishana mawazo juu ya majukumu yao katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani uliodumu kwa miongo mingi tangu Tanzania ipate uhuru hadi sasa.
Aidha, ziara ya Mhe. Haris nchini Tanzania inalenga katika kuunganisha nguvu za ushirikiano wa kimaendeleo kati ya nchi Tanzania na Marekani katika sekta za afya, kilimo, utalii, uchukuzi, uchumi wa buluu, mawasiliano, uchumi wa kidijitali, uungaji mkono hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na uhimilivu wake na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kupitia ubunifu, ujasiriamali na uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu ambazo Mhe. Haris na ujumbe wake watazitembelea ndani ya bara la Afrika kuanzia tarehe 25 Machi hadi tarehe 2 Aprili 2023. Nchi nyingine ni Ghana na Zambia.



