Thursday , 4th May , 2023

Picha ya vidio inayoonyesha droni ikilipuka juu ya Kremlin katika shambulio linalodaiwa kufanywa na Ukraine dhidi ya Rais wa Urusi imesambazwa Jumatano na mitandao kadhaa ya habari. Huku Ukraine ikikanusha shutuma hizo

Video hiyo inaonyesha kifaa kinachoruka kikirabia kuba ya jengo la baraza la Seneti katika Kremlin, na kulipuka kabla ya kulifikia. Urusi imeituhumu Ukraine kuishambulia Kremlin kwa droni usiku wa kuamkia Jumatano, katika jaribio lililofeli la kumuuwa Rais Vladmiri Putin, shutuma ambazo Kyiv imekana.

Rais Putin hakuwepo Kremlin wakati shambulio hilo likitokea, ambapo msemaji wake Dmitry Peskov ameliambia shirika la habari la serikali ya Urusi Ria Novosti, kwamba rais huyo alikuwa katika makazi yake ya Novo-Ogaryovo, nje ya Moscow.

Hata hivyo hakukuwa na uhakiki huru wa shambulio hilo ambalo maafisa wa Urusi wanasema lilitokea usiku lakini bila kuwasilisha ushashidi kuthibitisha madai hayo. Na wala maafisa hao hawakusema kwanini imechukuwa zaidi ya masaa 12 kuripoti tukio hilo.

Mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyask amekanusha ushiriki wowote katika tukio hilo linalodaiwa kuwa ni shutuma kubwa zaidi ambayo Urusi imetoa dhidi ya Ukraine tangu kutuma wanajeshi kuivamia nchi hiyo jirani zaidi ya miezi 14 iliyopita.