Thursday , 27th Jul , 2023

Umoja wa Wamiliki wa Vituo Vya Mafuta Tanzania (TAPSOA) wamesema kutokana na foleni kubwa katika upakiaji wa mafuta katika maghala mbali mbali nchini wanafanya kila jitihada kuhakikisha vituo vya mafuta vinapata nishati hiyo bila kuchelewa.

TAPSOA wamesema, 'Tutoe shukrani za dhati kwa taasisi mbalimbali, kama EWURA, wizara ya Nishati na taasisi nyingine za serikali kwa kuweka utaratibu wa kupakia mafuta kwa masaa ya ziada, zikiwemo pia siku za Jumamosi na Jumapili, ili kupunguza msururu wa magari yaliyojazana kwenye maghala mbali mbali ya mafuta nchini' 

Kwa kiwango kikubwa, magari mengi yamekua yanapakia mafuta usiku na mchana, ili kuepusha taharuki ya kukosa mafuta. Pia TAPSOA wanawashukuru wenye maghala ya mafuta yaani OMC's ambao wamekuwa na ushirikiano wa karibu katika kumaliza hizi changamoto kwa wakati na kwa haraka.

TAPSOA wamesema, 'Tunaendelea kuwasihi wanachama wa TAPSOA, na wateja wetu katika vituo vya mafuta wasiwe na taharuki, na mpaka sasa jitihada zinaendelea vizuri na magari yanaedelea kupakia katika maghala mbalimbali. Kutokana na jografia pana ya nchi yetu, kwa baadhi ya maeneo huenda kukawa na ucheleweshwaji kwakuwa magari yapo njiani kupeleka mafuta vituoni lakini tunafanya kila jitihada za msingi kusiwe na eneo litalokaukiwa kutopata mafuta' - TAPSOA.

Aidha, Serikali pia imewapa maelekezo wenye maghala ya mafuta (depots) kufanya kazi masaa 24 kuhakikisha foleni za magari yaliyopo katika maghala zinapunguzea kwa kupakia kwa wingi ili magari yawahi kupeleka mafuta vituoni.

Mnamo tarehe tarehe 23 Mwezi Julai Wamiliki wa maghala ya Mafuta na waagizaji wa mafuta waliihakikishia serikali na Wananchi kwamba wanayo mafuta ya kutosha kwa ajili ya kuwahudumia Wananchi.