Sunday , 5th May , 2024

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Wakunga na wataalamu wengine wa afya nchini kufanya kazi kwa weledi na kuongeza bidii katika kutoa huduma kwa wananchi wanaowahudumia.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Amesema kuwa kada zote za afya zinasimamiwa na miiko na maadili ya taaluma na miongozo iliyowekwa. "Hivyo basi kila mmoja ahakikishe anazingatia maelekezo mahsusi ya utendaji wa kazi."

Ameyasema hayo leo Jumapili, 5 Mei, 2024, alipokuwa mgeni rasmi katika Siku ya Mkunga Duniani na Mkutano Mkuu wa Chama cha Wakunga uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Chama cha Wakunga kiwe mstari wa mbele katika kukemea baadhi ya Wakunga wanaofanya kazi kinyume na maadili ya taaluma zao.

Majaliwa ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu na mazingira ya kutolea huduma ikiwemo kujenga majengo mapya, kufanya ukarabati wa majengo ya zamani na kujenga nyumba za watumishi karibu na vituo vya kutolea huduma ili kuhakikisha watoa huduma wanapatikana wakati wote. 

"Serikali imeweka juhudi kubwa katika kununua vifaa tiba, dawa, pamoja na magari ya kusafirisha wagonjwa ili kurahisisha rufaa kati ya vituo vya kutolea huduma na wakati inapotokea dharura," amesema Waziri Mkuu

Aidha, amesema maboresho hayo yamezingatia sana sehemu za kutolea huduma za mama na mtoto na kuhakikisha kuwa wodi za watoto wachanga na wale wenye matatizo (Neonatal Intensive Care Units) zinajengwa kwenye hospitali za Mikoa,Wilaya na baadhi ya vituo vya afya.