
Fadlu Davids
Msimu wake wa kwanza 2024/25 ameiongoza Simba kucheza fainali Kombe la Shirikisho barani Afrika na kupoteza mbele ya RS Berkane huku wakiishia hatua ya nusu fainali Kombe la CRDB baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Singida Black Stars.
Simba SC chini ya Kocha Fadlu inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC kwa tofauti ya alama moja dhidi ya vinara Yanga SC ambao watakutana Juni 15 kwenye mchezo wa Ligi namba 184. Simba akishinda mchezo huo atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutwaa taji hilo ambalo amelikosa kwa misimu mitatu mfululizo.
Ingawa msimu huu ni msimu wa kwanza kwa Fadlu ndani ya ardhi ya Tanzania lakini amefanikiwa kuonyesha makucha yake licha ya aina ya wachezaji aliowakuta katika kikosi hicho kutokuwa na muunganiko mkubwa kwasababu asilimia kubwa ya wachezaji wa kikosi hicho ni wapya.
Msimu ujao Simba tayari wamekata tiketi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika mpaka sasa wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu ya NBC, mashabiki wa Simba wakisubiri kwa hamu kuona mwenendo wa timu yao katika mashindano hayo makubwa Afrika