Monday , 28th Jul , 2025

Baada ya timu ya taifa ya wanawake ya England, kuandika historia nyingine ya kutwaa taji EURO kwa mara ya pili mfululizo mbele ya Uhispania, naomba nikudokeze baadhi ya mambo muhimu ambayo pengine huyafahamu katika mchezo huo yaliyoibua hisia ya mamilioni ya watu ulimwenguni.

Mosi mlinda mlango wa England, Hannah Hampton, mwenye umri wa miaka 24, amebeba historia ya kusisimua kwani alipokuwa mtoto alipokea taarifa kuwa hawezi kucheza soka kutokana na matatizo makubwa ya macho hali iliyopelekea afanyiwe upasuaji mara kwa mara. Hata hivyo Hannah Hampton, hakukata tamaa katika ndoto yake na hapo jana amefanikiwa kuokoa mikwaju miwili ya penati na kuisaidia timu yake ya taifa kubeba taji hilo.

Pili ni mshambuliaji wa England, Chloe Kelly, ambaye katika mchezo huo amefunga penati ya ushindi, ameandika historia ya kipekee kwani imepita miezi sita tu tangu alipoachwa na klabu ya Manchester City kutokana na kukosa nafasi ya kucheza. Baada ya hapo Chloe Kelly allijiunga na Arsenal ambapo alishinda kombe la UEFA, hatua ambayo ilimrejesha kikosini na kumpa nafasi ya kung’ara katika fainali ya EURO 2025. na sasa penalti yake ya mwisho ilihitimisha ushindi na kuhakikisha England inabeba kombe hilo kwa mara nyingine.

Wakati hayo yakiendelea mchezaji chipukizi Michelle Agyemang mwenye umri wa miaka 19 ametunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Mashindano. Michelle Agyemang, ambaye aliwahi kuwa kuchukua tuzo ya ball girl katika viwanja vya England, sasa ameandika historia kama mwanamke wa kwanza mweusi kushinda tuzo binafsi kwenye mashindano ya makubwa ya wanawake barani ulaya.