Thursday , 31st Jul , 2025

Makosa hayo yanadaiwa kutendeka kati ya Januari 2023 hadi Julai 17, 2025, katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza.

Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza leo Julai 31,2025 wakikabiliwa na jumla ya mashtaka matano yanayohusiana na uhalifu wa kiuchumi, likiwemo kosa la kuongoza genge la uhalifu na kukutwa na noti bandia.

Washitakiwa hao ni Richard Jackson Sinkala (38) mkazi wa Buhongwa, Hassan Ibrahim (47) mkazi wa Igoma, Emmanuel Simon Ngama (32) mkazi wa Nyahong’homango, na Gerald Melijory Majaliwa (30) mkazi wa Buhongwa, Jijini Mwanza. Wamefikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mhe. Erick Malrley, na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali Sileo Mazullah.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kosa la kwanza linawahusisha wote wanne kwa kuongoza genge la uhalifu, kukutwa na noti zilizoghushiwa, kosa la tatu linamhusu mshtakiwa wa kwanza peke yake, ambaye anadaiwa kufoji noti pamoja na kosa la nne la utakatishaji wa fedha huku kosa la tano likiwahusu washtakiwa wote wanne kwa tuhuma za utakatishaji wa fedha.

Makosa hayo yanadaiwa kutendeka kati ya Januari 2023 hadi Julai 17, 2025, katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza.

Baada ya kusomewa mashtaka yao, Hakimu Erick Malrley amewataka washtakiwa kutojibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi hiyo mpaka kibali kitakapowasilishwa, hivyo wamerejeshwa  Gereza la Butimba hadi Agosti 13, 2025, kesi itakapotajwa tena.