
Bio, ambaye alichukua uenyekiti wa ECOWAS mwezi Juni, amekutana juzi Jumanne na kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso Kapteni Ibrahim Traoré katika ikulu ya rais huko Koulouba.
Kulingana na ikulu ya Sierra Leone, Bio alijitolea kukuza uhusiano wa karibu na ushirikiano kati ya ECOWAS na muungano wa Sahel wakati wa ziara hiyo ya siku moja ambapo aliapa kuhakikisha kwamba amani inarejea Burkina Faso. Katika video iliyowekwa kwenye X ya Rais Bio alisema "Niko hapa leo kuonyesha mshikamano wangu na watu wa Burkina Faso, kuwaambia hawako peke yao na kwamba tutashirikiana kurejesha amani."
Haya yanajiri baada ya uhusiano wa mvutano kati ya kizuizi cha AES na ECOWAS - Mataifa ya Afrika Magharibi yanayoongozwa na serikali ya Niger, Mali na Burkina Faso kujiondoa rasmi kutoka kwa umoja wa kikanda unaojulikana kama ECOWAS mnamo Januari mwaka huu.
Vyombo vya habari vya serikali nchini Burkina Faso viliripoti kuwa mazungumzo hayo yaligusia usalama wa kikanda na uhusiano wa kimataifa huku wachambuzi wakisema kuwa safari hiyo inaonyesha kukubalika kwa umoja huo uliojitenga.
Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii, Bio alimshukuru Traoré kwa ukarimu wake. "ECOWAS daima imekuwa na jukumu muhimu katika kukuza amani, usalama, na ustawi wa kiuchumi katika mataifa yetu," aliandika.
"Ninatazamia kwa hamu kuendelea kushirikiana na ndugu zetu nchini Burkina Faso tunapojitahidi kudumisha maadili haya muhimu ya pamoja." Aliongeza