Tuesday , 25th Nov , 2025

Sambamba na hatua hiyo, ameeleza juhudi za Tanzania katika kujenga kuta za bahari ili kulinda jamii za pwani dhidi ya kuingiliwa na maji ya bahari kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Tanzania imewasilisha taarifa kwa niaba ya nchi 54 za Kundi la Afrika katika siku ya mwisho ya Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-30) jijini Belem, Brazil.

Taarifa hiyo imewasilishwa na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN), Dkt. Richard Muyungi, ambaye pia ni Mjumbe Maalum na Mshauri wa Rais katika masuala ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Afrika inasisitiza utolewaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutoka nchi zilizoendelea si hisani bali ni wajibu. Bara hilo linaendelea kusukuma mbele masuluhisho yanayolinda jamii, maisha na kufungua maendeleo endelevu kwa zaidi ya watu bilioni moja.

Dkt. Muyungi amesema ufadhili wa masuala ya hali ya hewa ni lazima utolewe kama ruzuku badala ya mikopo, akibainisha kuwa mikopo inaongeza mzigo wa madeni kwa mataifa ya Afrika. Alisisitiza kuwa Mfuko mpya wa Hali ya Hewa Duniani lazima utoe haki, usaidizi wa haraka na upatikanaji wa rasilimali kwa mataifa ya Afrika.

Katika hatua nyingine, Dkt. Muyungi amebainisha kuwa Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Kituo cha Mtandao cha Santiago mwaka 2025, ambacho kitaratibu msaada wa kiufundi kuhusu hasara na uharibifu.

Sambamba na hatua hiyo, ameeleza juhudi za Tanzania katika kujenga kuta za bahari ili kulinda jamii za pwani dhidi ya kuingiliwa na maji ya bahari kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wakati huo huo, AGN imeipongeza Ethiopia kwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa COP32 unaotarajiwa kufanyika Desemba 08–19, 2027, katika Jiji la Addis Ababa. Itakumbukwa kuwa mkutano kama huo uliwahi kufanyika Afrika katika mji wa Sharm el-Sheikh mwaka 2022.

Hivyo, Dkt. Muyungi alisema kuwa kukaribisha COP32 katika ardhi ya Afrika kwa mara nyingine tena kunathibitisha dhamira isiyoyumba ya bara hilo katika kuendeleza malengo ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) pamoja na Mkataba wake wa Paris.

Mkutano wa COP30 uliendeshwa chini ya kaulimbiu: “Dira 2050: Utekelezaji wa Hatua Jumuishi za Uhimilivu, Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo Endelevu.”