Wednesday , 17th Jun , 2026

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza wajumbe 11 wa kamati maalumu ya Kamati Kuu itakayoratibu na kuendeleza mchakato wa ukusanyaji wa maoni kuhusu upatikanaji wa katiba mpya kabla ya mwaka 2027.

Makada wa Chadema, John Heche, Mwanasheria Mkuu wa Chadema Rugemeleza Nshala pamoja na kada mwingine Boni Yai

Hatua hiyo inalenga kuchochea mjadala wa kitaifa na kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia maboresho ya mfumo wa kikatiba.

Kamati hiyo inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk. Rugemeleza Nshala, akiwa mwenyekiti, huku Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Wakili Deogratius Mahinyila, akiteuliwa kuwa katibu. Kamati imepewa hadidu za rejea nne na muda wa miezi mitatu kutekeleza majukumu yake.

Wajumbe wengine ni pamoja na Wakili Ali Ibrahim, Suzan Lyimo, Ruthy Moleli, Pamela Maasay, Wakili Gaston Garubindi, Zeud Mbano na Boniface Jacob maarufu Boni Yai.

Pia kamati hiyo imejumuisha washauri wawili wasio wanachama wa Chadema, ambao ni Wakili Mpale Mpoki na Wakili Jeremia Ntobesia, kwa ajili ya kuimarisha mchango wa kitaalamu katika mchakato huo.